emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa

Jisajili, Tukutambue, Tukutambulishe


NIDA YAENDELEA NA MABORESHO YA HUDUMA

NIDA YAENDELEA NA MABORESHO YA HUDUMA 

Na. Calvin Minja

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaendelea na juhudi za kuboresha upatikanaji wa huduma katika Ofisi zake za Wilaya pamoja na huduma za kidijitali ambazo zinamuwezesha mwananchi kujihudumia mwenyewe popote alipo kirahisi na kwa wakati. 

Maboresho haya yanajumuisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA ambayo inaongeza ufanisi na uwazi katika upatikanaji wa huduma, ongezeko la vituo vya utoaji huduma katika maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu, pamoja na kuwapatia mafunzo ya mifumo ya kisasa ya ili waendelee kutoa huduma bora kwa wananchi.

Katika maboresho yanayoendelea ya upatikanaji wa huduma, NIDA imefungua vituo vya utoaji huduma katika Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwemo Kituo cha Huduma Jumuishi kilichopo Mnazi Mmoja jengo la Anatoglo, Kituo cha Huduma Pamoja kilichopo jengo la Posta Mpya, pamoja na kituo kingine kilichopo Viwanja vya Mwalimu Nyerere maarufu kama Sabasaba. Vituo hivi vimeanzishwa ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kupunguza msongamano kwenye Ofisi za Wilaya.

Katika upande wa TEHAMA, NIDA imeanzisha mfumo wa usajili, ambapo mwombaji anaweza kujaza taarifa zake za awali yeye mwenyewe kwa njia ya mtandao kwa wale wanaojiandikisha kwa mara ya kwanza. Kupitia kiunganishi wezeshi https://eonline.nida.go.tz, mwananchi anaweza kujaza taarifa zake binafsi kwa usahihi, hatua hii inapunguza makosa ya taarifa pamoja na muda wa kusubiri pindi mwombaji anapofika ofisini kwa ajili ya usajili kabla ya hatua za mwisho za uchukuaji wa alama za kibaolojia. Mfumo huu umerahisisha mchakato mzima wa usajili na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Kupitia maboresho hayo, NIDA imehakikisha kuwa Namba ya Utambulisho wa Taifa inapatikana ndani ya kipindi cha wiki moja baada ya usajili kukamilika. Mwananchi atapokea ujumbe mfupi (SMS) kwenye namba ya simu aliyojaza kwenye fomu ya maombi ya utambuisho. Aidha, baada ya kupata namba hiyo, mwananchi ataweza pia kupata taarifa za Kitambulisho chake kama kipo tayari kupitia namba ya simu iliosajiliwa kwa namba yake ya NIDA. Hali hii imepunguza msongamano usio wa lazima kwenye Ofisi za NIDA za Wilaya na kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Kwa upande wa huduma za kidijitali, NIDA imeboresha upatikanaji wa huduma kwa njia ya mtandao. Maboresho haya yanajumuisha uboreshaji wa Self-Service Portal, inayopatikana kupitia kiunganishi wezeshi https://services.nida.go.tz. Kupitia kiunganishi hicho, wananchi wanaweza kufuatilia maendeleo ya maombi ya Namba ya Utambulisho wa Taifa pamoja na kupata Namba ya Malipo ya Serikali kwa huduma zinazohitaji malipo, kama vile upotevu wa kitambulisho na mabadiliko ya taarifa za usajili, kuwasilisha maombi ya usajili kwa urahisi, kufuatilia maendeleo ya maombi yao kwa wakati wowote na kupata taarifa muhimu bila ya kulazimika kufika ofisini.

Vile vile, NIDA imeimarisha huduma kwa wateja kwa kuongeza ufanisi wa kupokea na kujibu maswali, malalamiko au maombi ya wateja kupitia njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo namba ya simu 023 221 0500, barua pepe info@nida.go.tz, au mitandao ya kijamii ya Mamlaka. Ikiwemo Instagram, Facebook na X. Maboresho haya yameongeza kasi ya majibu, uwazi katika utoaji wa taarifa na kurahisisha ufuatiliaji wa maombi.

Kadhalika, NIDA imeongeza nguvu katika kampeni za elimu kwa umma kwa kushiriki kikamilifu katika maonesho ya kitaifa, makongamano na mikutano ya kijamii ili kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa sahihi wakati wa usajili, athari za taarifa zisizo sahihi, na taratibu za kurekebisha taarifa endapo kutatokea makosa. Elimu hii inalenga kuongeza uelewa wa wananchi ili kupunguza changamoto zinazojitokeza baada ya usajili.

NIDA inawahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Mamlaka kwa kutoa taarifa sahihi, kufuatilia huduma kupitia njia rasmi na kuzingatia taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata Kitambulisho cha Taifa chenye taarifa sahihi kwa wakati na uwazi.

UCHAGUZI MKUU OKTOBA 29, 2025

Kura Yako Haki Yako Jitokeze Kupiga Kura