emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa

Jisajili, Tukutambue, Tukutambulishe
Usajili na Utambuzi wa Raia

Jinsi ya kujaza fomu ya Usajili kwa raia:-

Jaza fomu ya maombi ya Utambulisho wa Taifa Namba 1A kwa kalamu ya wino mweusi na kwa herufi kubwa. (Fomu inapatikana kwenye ofisi ya Usajili ya NIDA, Wilayani/Serikali ya Mtaa na kwenye tovuti yetu)

 fomu ya maombi ya Utambulisho wa Taifa Namba 1A

Hakikisha una saini fomu yako ya maombi ya Utambulisho wa Taifa kwenye kipengele Namba 59/60 ama umeweka alama ya dole gumba iwapo hauna saini rasmi ama hujui kusoma na kuandika,

Gonga muhuri fomu yako ya Maombi ya Utambulisho wa Taifa kwenye Serikali ya Mtaa unakoishi kipengele namba 59/60 na kuandikiwa barua ya utambulisho wa makazi,

Ambatisha nyaraka zifuatazo, viambatisho hivi ni vya lazima:
    i.   Cheti cha kuzaliwa,
    ii.  Barua ya utambulisho wa makazi kutoka Serikali ya Mtaa unakoishi,
    iii. Cheti cha kuzaliwa au Kitambulisho cha Taifa cha mzazi mmoja.

Ambatisha viambatisho vya ziada ulivyonavyo kati ya vifuatavyo:
    i.  Vyeti vya Masomo-Msingi,Sekondari,Chuo,
    ii.  Pasi ya kusafiria,
    iii. Leseni ya udereva,
    iv. Namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN),
    v.  Kadi ya bima ya afya,
    vi. Kitambulisho cha mzanzibar mkaazi

Wasilisha fomu yako ya maombi kwenye Ofisi ya Usajili ya NIDA wilaya unakoishi kwa ajili ya kuchukuliwa alama za kibaiolojia (kupigwa picha, kuweka saini ya kielektroniki na kuchukuliwa alama za vidole) ili kupisha hatua zinazofuata ziendelee.

Mavazi ya kuzingatia wakati wa Usajili: Ili picha ya mwombaji wa Utambulisho wa Taifa itoke katika ubora uliokusudiwa pindi unapowasilisha fomu ya maombi kwenye ubalozi husika kupigwa picha na kuchukuliwa alama za vidole, unashauriwa kutovaa nguo; nyeupe, kijivu, bluu mpauko, pinki au nguo za kung’aa, jezi, nguo zenye nembo, michoro au maandishi, kofia aina yoyote na kutopaka hina viganjani ili alama za vidole zisomeke kirahisi,

Hatua mbalimbali za usajili na utambuzi wa watu:-
    i.  Ujazaji wa fomu za Utambuzi na Usajili,
    ii. Uhakiki wa awali wa fomu za maombi,
    iii. Uingizaji wa taarifa kwenye mfumo wa kompyuta,
    iv. Kuthibitishaji taarifa za mwombaji zilizo katika mfumo wa kompyuta,
    v.  Uchukuaji wa alama za vidole, picha na saini ya kielektroniki,
    vi. Utengenezaji wa Daftari Kuu la Taarifa za Watu,
    vii. Uhakiki wa mwisho,
    viii.Uchapishaji, uhakiki wa ubora na Utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.

Ufafanuzi wa mambo msingi hitajika kwa baadhi ya hatua za usajili tajwa hapo juu;

1.1.1. Usajili – Ujazaji wa fomu (biographic data)

Mwombaji wa Kitambulisho Raia, Mgeni ama Mkimbizi anatakiwa kufika katika kituo/ofisi ya usajili na vivuli (Copy) ya nyaraka za kutambulisha makazi, uraia na umri wake kama ilivyoainishwa hapo juu katika kipengele cha mahitaji ya kila kundi wakati wa usajili.

1.1.2. Uchukuaji alama za kibaiolojia

Hatua hii ya Usajili inajumuisha upitiaji wa taarifa za mwombaji katika mfumo, uchukuliwaji wa alama za vidole, picha na utiaji wa saini ya kielektroniki ambapo kuna mambo msingi ya mwombaji kuzingatia ambayo ni;

Kwa ajili ya ubora na mwonekano mzuri wa picha mwombaji unashauriwa kutovaa nguo nyeupe, pinki, kijivu, bluu mpauko au nguo zenye rangi za kungaa sana. Kutovaa kofia ya aina yoyote wakati wa kupiga picha, au kupaka hina viganjani wakati wa uchukuaji wa alama za kibaiolojia.

Ili kurahisisha zoezi hili, mwombaji unaombwa kufika kwenye ofisi/kituo cha usajili na nyaraka halisi (original) za kuthibitisha uraia na umri wake mathalani, cheti cha kuzaliwa, pasipoti, vyeti vya elimu ya msingi na sekondari, leseni ya udereva, kitambulisho cha bima ya afya, kitambulisho cha mpigakura na kitambulisho cha mzanzibar mkazi.

1.1.3. Uhakiki na Uwekaji Pingamizi

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika hatua hii inakuwa ikiendesha zoezi la kupokea maoni ya uwekaji pingamizi kutoka kwa wananchi juu ya wakazi waliofanya maombi ya kupatiwa Vitambulisho vya Taifa na Uhakiki wa mwisho wa taarifa za waombaji kabla ya kuanza uchapaji na ugawaji wa Vitambulisho kwa wakazi ambao wamekamilisha hatua ya kuchukuliwa alama za kibaiolojia (picha, alama za vidole na saini ya kielektroniki).

NIDA kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mitaa, vyombo vya usalama na wananchi kwa jumla inakuwa ikipokea taarifa za maoni au pingamizi kuhusiana na waombaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wakazi wa maeneo husika. Hii ni hatua muhimu katika kutekeleza azma ya Serikali ya kujenga mfumo madhubuti wenye taarifa na kumbukumbu sahihi za watu, hivyo wananchi wanaweza kutoa pingamizi la kimaandishi wakieleza sababu ya pingamizi kwa kuainisha upungufu ambao wamebaini, mathalani taarifa za URAIA, UMRI, MAJINA, PICHA na MAKAZI ya mwombaji kwa kujaza fomu maalum kwenye mtaa husika au kutoa taarifa NIDA kwa kutuandikia barua kupitia anuani S.L.P 12324 Dar es Salaam, barua pepe, au kuziwasilisha kwenye Ofisi za wilaya husika.

NIDA inawaomba wananchi kuwa wazalendo na kujitokeza kuhakiki taarifa zao na waombaji wengine, na kutoa pingamizi bila upendeleo, uonevu au kukomoana.

1.1.4. Ugawaji Vitambulisho vya Taifa

Mwombaji anatakiwa kufika katika ofisi ya usajili katika wilaya husika ama kulingana na maelekezo/matangazo yanayotolewa katika eneo hilo ili kupatiwa kitambulisho chake kwa kuzingatia kuja na risiti maalumu aliyopatiwa na NIDA wakati alipokamilisha kuchukuliwa alama za kibaiolojia.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali fika kwenye Ofisi ya Usajili ya NIDA Wilayani au wasiliana na NIDA kupitia Namba: 0752 000 058, 0687 088 888, 0777 740 006, 0677 146 666. Tovuti www.nida.go.tz, Barua pepe info@nida.go.tz, Facebook, Instagram, Twitter Nidatanzania

Jisajili, Tukutambue, Tukutambulishe!